Na Amrat Kombo, Zanzibar
Dunia ni darasa la kujifunza mengi,
mazuri na yenye machungu na mengine humuacha mtu anajiuliza masuali ambayo
jawabu yake haipati na kila akiona anaikaribia hopotea kama moshi hewani.
Uzoefu umetuonyesha kwamba kukosa na
kupata ni majaaliwa, lakini badhi ya watu hujiengea dhana na kuiamini
hata kufikiria yupo mtu au kikundi cha watu ndio kikwazo cha kwake yeye kupata
maendeleo.
Hapo zamani wazee wetu
walishikana mikono, wakasafishiana nyoyo zao na kusaidiana kwa hali na mali,
iwe wakati furaha au wa shida. Lakini sasa mambo yamebadilika, nguvu ya pesa
imechachamaa.
Kila mtu masikini anapojaribu
kujipapatua anakuta anapanda mlima ambao kilele chake hakioni. Yote haya
yametokana na wengi wenye mamlaka na madaraka kutojali shida za mtu
masikini .
Katika kutaka kujuwa juhudi za
wanawake kutaka kushika nafasi za uongozi ili wasaidie wanawake wezao watokane
na umasikini nilikwenda Kikungwi, mkoa wa Kusini Uguja.
Huko nilikutana na mwanamama
mcheshi, mkarimu, jasiri na mchapa kazi, mwenye rangi ya jongoo na sura nzuri
ya duara na umbile lenye haiba ya mwanamke aliyenieleza mengi juu ya safari
yake ya kugombea uongozi.
Bahati Issa Suleimani, mwenye umri
wa miaka 51 , mwenye watoto 6 alithubutu kuwania nafasi mbalimbali za uongozi,
ikiwemo ya katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) katika mwaka 1995,
na Mwenyekiti wa Umoja Wanawake Tanzania mnamo mwaka 2017.
“Katika mwaka 2020 niligombea nafasi
ya udiwani, lakini kwa bahati mbaya sikufanikiwa, sikukata tama.
hivyo niligombea tena nafasi ya Mwenyekiti Wanawake Tanzania (UWT) wa
jimbo mwaka 2023 ila sikufanikiwa’’,alielezea.
Kukosa huko hakukumkatisha
tama Bahati kwa kuamini iposiku atafanikiwa.
Amesema ilimsikitisha kuwa sasabu ya
kutofanikiwa ni kuona kilichothaminiwa katika hizo chaguzi ni pesa na sio utu
na uwezo wa mtu.
‘’ Umaskini wangu ndio uliopelekea
nikose nafasi kwani baadhi yawananchi waliona siwezi kuleta maendeleo kwakuwa
sina pesa ,hivyo wakaona bora wasinipigie kura.”ameongezea
Alichobaini ni kuwa jamii
iliyomzunguka ina mtazamo hasi juu ya wanawake kushiriki katika siasa na
jambo la kushangaza ni kuona wanawake wenzake waliokuwa mstari wa mbele
kumkandamiza.
“Ukiangalia nafasi ya udiwani
wagombea tulikuwa 6 wanaume watano na mwanamke nilikuwa peke yangu na kwa
nafasi ya ubunge wagombea wote watatu walikuwa wanaume. .”Amesema
Bahati ameniambia anaona ni vyema
vyama vya siasa vikachukua juhudi za kuwainua wanawake kiuchumi ili hatimaye
wawe na nguvu ya kugombea uongozi.
Safari haikuishia kwa
Bahati tu niliendelea kusonga mbele hadi Kombeni na kukutana na Aisha
Haji Mzee aliethubutu kuwania nafasi ya uwakilishi katika Jimbo la
Mwanakwerekwe.
" Katika mwaka 2020 nilithubutu
kugombea uwakilishi katika Jimbo la Mwanakwerekwe lakini sikufanikiwa
kupata aliongea kwa masikitiko huku akitikisa kichwa."
Alisema kukosa fedha ndio
kikwazo kilichopelekea kushindwa kwake, kwani hakua na uwezo wa kupiga kampeni
,kuandaa mikutano na kuwafikia watu kwa wakati. ingawa chama kilimsaidia
lakini kilishiwa njiani kutokana na hali duni ya chama hicho. amesema
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa chamacha
Adatadea Ali Makame Issa, amesema ukosefu wa Ruzuku kwa baadhi ya
vyama vya siasa ni sababu kubwa ya kushindwa kusaidia wanawake kushika
nafasi za uongozi.
“Ili chama kiweze kumsaidia wanawake kuingia kwenye nafasi ya uongozi kinatakiwa kiwe na Ruzuku ambayo itakayoweza kutatua changamoto wanayokabiliana nayo.”Amesema
Katibu Mkuu wa Chama cha Makini,
Ameir Hassan Ameir, amesema bado chama chao ni kichanga na
hakina vyanzo vya mapato ambavyo vingeweza kupunguza tatizo hilo, alipendekeza
serikali itowe ruzuku maalum kwa wagombea wanawake ili kuwasaidia
kutimiza malengo.
Ushauri huo umenifanya nitembelee
ofisi ya msemaji wa serikali Hamza Hassan Juma ambae ni waziri wa nchi
ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar na kueleza kuwa serikali inatoa
ruzuku kwa kufuata sheria.
" Kifungu cha 16 cha sheria ya
vyama vya siasa hairuhusu kila chama kupewa ruzuku isipokuwa chama ambacho kina
uwakilishi ndani ya Baraza la Wawakilishi, au chama ambacho kimepatakura
nyingi." Amesema
Hata hivyo, amesema ruzuku sio
sababu ya kuwazuia vyama vya siasa kusaidia wanawake kuingia katika uongozi kwa
sababu vyama vya siasa vinatakiwa kutoa michango katika matawi yao ili kusaidia
shughuli za kisiasa.
“Serikali haitoi ruzuku kwa vyama
visivyotimiza vigezo vya kupewa Ruzuku kama vile kuwa na wanachama wachache wa
kuweza kuwaweka viongozi wao katika chombo cha kutunga sheria ”Amesema
Hata hivyo, zipo taasisi zinazohamsisha
wanawake kujikomboa kiuchumi kwa lengo la kuwasaidia katika harakati za
kisiasa .Katika Idara ya Maendelao ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto niliongeana
na mkurugezi wa idara hiyo, Siti Abasi Ali, Amesema
Wamehamasisha vikundi mbalimbali vya
wajasiriamali wanawake kuchukuwa mikopo isiyo na riba ya viko 19 ambayo
itawasaidia kuimarika kiuchumi na kuwajengea uwezo katika shughuli zao za
kisiasa.
“Tumepata vikundi vya wajasiriamali
wanawake 1,971 vikiwa na wanawake 59,753 lengo ni kuhamasisha wanawake waweze
kufanya biashara ili kuhakikisha wanapata fedha ambayo itawainua kiuchumi
katika kugombea nafasi za uongozi.
Amewashauri wanawake
kuchangamkia fursa za mikopo iliyopo ili kuwasaidia katika shughuli zao za
kimaendeleo na kisiasa.
Chama cha Waandishi wa Habari
Wanawake Tamwa – Zanzibar kinatoa mafunzo ya uongozi kwa wanawake na
kutatua changamoto zinazowakabili.
Mkurugenzi wa Chama hicho
Dkt.Mzuri Issa alikiri kwa masikitiko kwamba wanawake wengi wamekumbana na
changamto walipotaka kugombea uongozi.
“Tumetoa mafunzo ya uongozi kwa wanawake kwa kushirikiana na Jumuiya ya wanasheria wanawake Zafela na zidi ya wanawake 100 tumewapatia mafunzo hayo Unguja na Pemba. Tulichogungundua ni asilimia 50 ya wanawake wamekutana na changamoto ya uchumi.”Amesema
Ukiangalia wawakilishi wa majimbo 50
Zanzibar wanawake 8 sawa na asilimia 16,wabunge wa jamuhuri ya muungano kutoka
Zanzibar kwenye majimbo 50 wanawake wanne ,sawa na asilimia 8 mawaziri 6
sawa na asilimia 33,makatibu wakuu 7 sawa na asilimia 39.
Kwa upande wa wakuu wa mikoa
mwanamke mmoja sawa na asilimia 20,wakuu wa wilaya wanne sawa na
asilimia 36 na masheha wanawake 79 sawa na asilimia 20, wanaume 309 sawa na
asilimia 80 kwa masheha wote wa Unguja na Pemba ambao ni 388.
0 Comments