Ticker

6/recent/ticker-posts

Watumishi Wa Umma Watakiwa Kuwa Mstari Wa Mbele Kutetea Haki Za Watu Wenye Ulemavu

Na Amrat Kombo:

Watumishi wa umma nchini wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuwalinda na kuwatetea watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kufikia maendeleo na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Watu Wenye Ulemavu, Ndugu Abeda Rashid Abdalla, wakati akiwasilisha mada kuhusu masuala ya watu wenye ulemavu katika mafunzo elekezi kwa watumishi wa umma kutoka taasisi mbalimbali za serikali, yaliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-Wakil, Kikwajuni.

Amesema kuwa ushiriki wa watumishi wa umma katika kutetea haki hizo ni muhimu kwa sababu unawasaidia watu wenye ulemavu kutekeleza vyema majukumu yao katika maeneo ya kazi na jamii kwa ujumla.

Abeda Rashid ameongeza kuwa licha ya juhudi za serikali katika kupigania haki za watu wenye ulemavu, bado baadhi ya taasisi za umma zina uelewa mdogo kuhusu haki na mchango wa kundi hilo muhimu. Ameeleza kuwa ni wakati sasa kwa taasisi hizo kubadilika na kutoa ushirikiano wa kutosha kila inapohitajika.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Mafunzo Mafupi wa Chuo cha Utawala wa Umma (IPA), Mwalimu Abdalla Juma, aliyefunga mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi wa chuo hicho, amewataka watumishi wa umma kudumisha nidhamu, mshikamano na upendo miongoni mwao ili kuhakikisha mafanikio katika maeneo yao ya kazi.

Nao watumishi wa umma walioshiriki mafunzo hayo wameahidi kuyafanyia kazi mafunzo waliyopewa ili kuleta mabadiliko chanya yenye maslahi kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments