Baadhi ya bidhaa zinazotengezwa na kikundi cha kuweka na kukopa cha Mwanzo Mgumu kilichopo Michamvi Kae |
Na Ahmed Abdulla, Zanzibar:
INAELEZWA kuwa ujio wa mradi wa kijaluba kumewasaidia wananchi
wengi walionufaika na mradi huo kuinua hali zao za kiuchumi pamoja na kupata
elimu ya utengenezaji wa bidhaa mbalimbali.
Mradi huo uliolenga ushirikishwaji wa kwatu
wenye ulemavu katika kukuimarisha hali za jamii uliakisi matakwa ya kuzingatia
usawa katika kutekeleza majukumu ya kujitafutia riziki za halali.
Wapo ambao kwasasa wanaweza kufanya kazi za
mikono ikiwa ni pamoja na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali ikiwemo
sabuni,mafuta ya kujipaka pamoja na mapambo.
Hii ni kutokana na mafunzo mbalimbali waliopatia
lengo kuu ni kuondoa utegemezi eti kwa kisingizio kuwa ni mwenye ulemavu.
Ramadhan Haji Vua ni Mwenyekiti wa kikundi cha
kuweka na kukopa Tutambuane kilichopo shehia ya Kikadini, Jambiani alisema moja
ya eneo lililowasaidia kwa kiasi kikubwa ni eneo la mfuko wa jamii.
“Tulipata maafa ya mvua kubwa, nyumba zikaingia
maji hivyo waliopata huo msiba wakafarijika na mfuko huu wa jamii ndio nikaona
huu mradi umetutoka gizani” alisema
Kwa upande wa bi Asha Amour kutoka kikundi cha
Nyota Ya Bahati chenye jumla ya wanachama 30 kilichopo Bwejuu Kusini Mwa Kisiwa
Cha Unguja alisemema ujio wa mradi huo umewafanya wakwamuke kwenye janga la
umasikini kwani baadhi yao wameanzisha biashara zilizotokana na kukopa fedha katik
vikundi vyao.
“Kuhusu kusomesha na matibabu hayanipigi chenga
hii ni kutokana na faida ninayoipata kwenye kikundi” alisema Bi Asha
Jee baada ya mkupuo wa kwanza wa ukusanyaji wa
hisa za vibubu vya Vikundi vinavyonufaika na mradi wa Kijaluba kuna hamasa
iliyoongezeka kwenye Vikundi hivyo?
Mohammed Haji Khamisi ni katibu wa kikundi cha
Tutambuane alisema kutokana na faida iliyopatikana kwenye mkupuo wa kwanza
kumetoa hamasa kwa wananchi kujiunga na kikundi chao hali iliyoifanya idadi
kuongezeka kutoka wanachama 25 hadi 30.
“Tunaendeleza kwa sababu tumeona mafanikio yake
jinsi gani tunavyojisaidia na ndio mana wanachama wameongezeka” Alisema
Kwa upande wa kikundi cha mwanzo mgumu kupitia
kwa mshika fedha wao Mwanahamis Shaes Khamis Alisema ni faraja kwao kuja kwa
mradi wa kijaluba kwani umewarahisishia kupata mikopo kwa wakati na isiyokuwa
na riba.
“Kila tulipoomba mikopo kwa ajili ya kuanzisha
biashara zetu tulikwama kwa sababu ya riba ila kuja kwa kijaluba sasa
tunakopa,tunafanya biashara na tunajiinua kiuchumi. Alisema
Kwa upande wake Afisa program kutoka chama cha
waandishi wa Habari Wanzawake Tanzania upande wa Zanzibar (TAMWA-ZNZ) Khairat
Haji alisema wanavikundi waliwapatia mafunzo mbalimbali ikiwemo ya kutambua
haki zao (watu wenye ulemavu), elimu ya kuweka na kukopa, umuhimu wa kuweka
akiba,jinsi ya kutumia mikopo na kufanya biashara, kutengeneza bidhaa pamoja na
mafunzo ya uendeshaji wa biashara.
“tumeona wengine wafunguwa biashara ya sabuni
sasa walipatiwa mafunzo ya jinsi ya kuendesha biashara ili ilete faida” alisema
Khairat
Aidha aliendelea kusema kuwa “tunashukuru lengo
limefanikiwa kwasababu wakati tunaanza ilikuwa ngumu kutokana na mitazamo ya
jamii kufikiria kuwa watu wenye ulemavu ni watu wa kupewa na sio mtu anateweza
kuweka kitu”
Khairat pia alisema ni jambo la kufurahisha
kuona wanajamii wanafurahia uwepo wa mradi huo na kuona tija ya vikundi vyao
inapatikana.
Mradi wa kijaluba ni wa miaka miwili ulianza
mwaka 2022 na unatarajiwa kukamilika Mwezi Oktoba mwaka huu na unatekelezwa na
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania upande wa Zanzibar (TAMWA-ZNZ)
na shirikisho La jumuiya za watu wenye Ulemavu Zanziba (SHIJUWAZA).
0 Comments