Ticker

6/recent/ticker-posts

Habari Za Wanawake Na Makundi Ya Watu Wa Pembezoni Zimeleta Mafanikio Katika Nchi


NA ASIA MWALIM:

CHAMA Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, TAMWA-Zanzibar kimesema, wanajivunia kuona wanawake wengi wamehamasika kushiriki katika masula ya uongozi kutokana na kupata elimu ya uongozi mara kwa mara inayotolewa na Chama hicho.

Mkurugenzi wa Chama hicho, Dk. Mzuri Issa aliyasema hayo katika mahafali ya Waandishi wa Habari Chipukizi (YMF) 24 , iliyoshirikisha wahariri na waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali huko ukumbi wa Bima, Mperani Mjini Unguja.

Alisema, Program za waandishi wa habari zimesaidia kuleta mabadiliko makubwa kwenye nchi kwa kufanya mageuzi maeneo bali mbali ikiwemo suala la sheria, na kuhamasisha wanawake wengi kujitoa kwenye mambo yanayowahusu.

Aidha aliwataka waandishi wa Habari vijana kuendelea kuandika habari za makundi ya pembezoni ili kuleta hamasa kwa wanawake kujitokeza zaidi kwenye uchaguzi mkuu wa 2025 kwenye ngazi mbali mbali.

Mjumbe wa Bodi ya TAMWA Zanzibar, Haura Shamte, aliwapongeza waandishi kwa kujitoa na kuonesha utendaji wao jambo ambalo limesaidia kutoa stori nyingi zinazowahusu wanawake.

Aliwataka waandishi hao kuendelea kuandika habari za Wanawake ili kuitendea haki taaluma hiyo kwa kufuata maelekezo na uweledi wakati wa kazi zao.

Muwakilishi wa Majaji wa kazi za waandishi wa habari vijana, Shifaa Saidi Hassan, aliwatka waandishi wa habari kuendelea kuutumia ujuzi huo kwa kazi zao sambamba na kutoa ujuzi huo kwa waandishi wa habari wengine ili kupata maendeleo nchini.

Aliwapongeza vijana walioshiriki katika mradi wa kuibua wanawake na uongozi kwani wameutendea haki, kufanya kazi nzuri, zenye ubora wa kushindanishwa na zenye maslahi ya jamii na nchi kiujumla.

Alieleza baadhi ya Changamoto zilizojitokeza wakati wa kuchuja kazi hizo ni kubaini baadhi ya waandishi kufanya mahojiano marefu, hivyo aliwasisitiza kuyafikia makundi ya pembezoni ikiwemo watu wenye ulemavu, wanawake na watoto ili sauti zao kusikika.

Alitaja idadi ya kazi zilizowasilishwa kufanyiwa mchujo ni 175, kati ya hizo makala za Magazeti 15, Redio 85 na mitandao ya kijamii, ambapo vigezo muhimu walivyoangalia ni weledi na umahiri katika sauti, umahiri wa lugha na upekee wa mada.

Kaimu Afisa Programmu TAMWA -Zanzibar Khairat Haji, alisema mradi wa kuimarisha uongozi kwa wanawake unatekelezwa kwa awamu ya pili ambao umewashirikisha waandishi wa habari vijana 24 wa Unguja na Pemba.

Alieleza kuwa hadi kufikia mahafali hiyo kazi 347 zimewasilishwa kutoka kwenye vyombo mbali mbali vya habari ambapo kati ya kazi hizo Makala za magazeti 47, Radio 117, Mitandao ya kijamii 187.

Baadhi ya wahariri waliofika katika sherehe hiyo, waliipongeza TAMWA kwa kazi kubwa ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari vijana, na kuiomba TAMWA Zanzibar kuwafikia wahariri wa vyombo mbali mbali ili kuendana na kasi ya teknolojia na uandishi unaoendana na wakati.

Nao wahitimu wa mafunzo ya Young Media Fellowship (YMF) walipongeza TAMWA kwa kuwapatia mafunzo hayo na  kuahidi kuendela kufanya kazi zao kwa uweledi ili kuibua matatizo ya jamii.

Katika sherehe hiyo waandishi wa habari vijana wametunukiwa vyeti vya kuhitimu na zawadi ya Computa kwa waandishi 3 waliofanya vizuri kupitia mradi huo uliofadhiliwa na Shirika la National Endowment for democracy (NED).

Post a Comment

0 Comments