RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa
shukurani zake za dhati kwa Jumuiya ya Zawiyyatul Qadiria - Tanzania
iliyomuombea dua Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi.
Al hajj Dk. Mwinyi alitoa shukurani hizo baada ya Ibada
ya sala ya Ijumaa iliyoambatana na dua maalum ya kumuombea Hayati Mzee Ali
Hassan Mwinyi, Rais mstaafu wa Zanzibar na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,
huko Masjid Ngamia Welezo, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Al hajj Rais Dk. Mwinyi alishukuru Jumuiya hiyo kwa
niaba ya familia yake, pamoja na kuwataka waumini wa dini ya Kiislam kuendelea kumuombea
dua Marehemu Mzee Mwinyi pamoja na kuliombea taifa ili liendelee kudumu kwenye
amani na utulivu.
“Tuendelee kumuombea dua Mzee wetu, tuendelee
kuiombea dua nchi yetu iendelee kudumu kwenye amani tuliyokuwa nayo na Mwenyezi
Mungu atupe wepesi katika majukumu yetu” Alisisitiza Al hajj Dk. Mwinyi.
Marehemu Mzee Ali Hassan Mwenyi alifariki dunia Febuari
29 mwaka huu, Dar es Salaam na kuzikwa Machi 02, 2024 Mangapwani, Mkoa wa
Kaskazini Unguja.
Akizungumza kwenye hafla ya dua hiyo, Kadhi Mkuu wa
Zanzibar, Sheikh Hassan Othman Ngwali mbali na kumpa pole Al haj Dk. Mwinyi kwa
msiba wa mzee wake uliotokea hivi karibuni lakini pia alitoa shukurani kwa
waislam wote waliohudhuria ibada ya sala ya Ijumaa pamoja na dua maalum ya
kumuombea Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi pamoja na kuiasa jamii kuongeza
ushirikiano kwenye masuala ya kijamii.
Naye Khatib wa ibada ya Sala ya Ijumaa, msikitini
hapo aliwataka waumini wa Kiislam kukithirisha sana ibada kipindi hiki cha
Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa kuendelea kusoma Quran tukufu, kutoa sadaka kwani
huweka wepesi wa wamchao Mola, pamoja na kushajihisha jamii kusaidiana kwa kufutarishana
hasa kwa wasiokuwa na uwezo kusaidiwa zaidi kipindi hiki.
Sambamba na kuueleza kwamba kila inapofika mwezi
Mtukufu wa Ramadhan Mwenyezi Mungu (S.W) huifungua milano yote ya Pepo na
kuifunga milango saba ya Moto pamoja na mashetani kufungwa ili kutoa fursa
nzuri kwa waumini wa kiislam kufanya ibada kwa uhuru.
Akitoa historia ya fupi ya Jumuiya ya Zawiyyatul
Qadiria – Tanzania, Mkurugenzi wa huduma nyenginezo wa Jumuiya hiyo, Sheikh
Siasa, alisema iliasisiwa mwaka 1988 Tanzania Bara na baadae mwaka 1992
lilifunguliwa tawi lake Zanzibar likiongozwa na mlezi wake Sheikh Said Othman
Abdul Kadir Othman bin Muhammed bin Nuur.
0 Comments