Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dokta Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuweka Sera na Mipango madhubuti ili kuimarisha Ustawi na Maendeleo ya Wazee wote Nchini.
Dokta Mwinyi ameyasema hayo leo katika Hotuba yake iliyowasilishwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, wakati wa Hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani, katika Ukumbi wa Dokta Shein wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema, kama ilivyokuwa dhamira ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964, chini ya Kiongozi Shupavu, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, iliyohakikisha inapelekea kuandaa Mipango imara ya kuitunza Sehemu na Rika hiyo Muhimu ya Jamii, Serikali inao wajibu wa kusimamia na kuona hayo yanaendelezwa.
Hivyo amesema, ni jukumu la kila mmoja kuungamkono jitihada za Serikali na Wadau wengine ili kuhakikisha hali, ustawi na hadhi ya Wazee Nchini inaimarika.
"Kwa mara nyengine tena, nazihimiza taasisi, mashirika na wadau, zikiwemo Jumuiya za Wazee Nchini, kuendelea kuungamkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha Zanzibar inaendelea kuwa ni mahala bora pa kuishi kwa watu wa rika zote", amehimiza Dokta Mwinyi.
Aidha, ameainisha jitihada mbali mbali za Serikali katika kujenga ustawi wa rika hiyo ikiwemo kuondoa ubaguzi; kuimarisha uwezo na kukuza ushiriki wa kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa makundi yote, bila ya kujali umri, jinsia, hali ya ulemavu, rangi, kabila, dini, mahali mtu anapotoka au hali yake ya kiuchumi.
Sambamba na hayo, Dokta Mwinyi ametaja Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya Mwaka 2050; na Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar (ZADEP 2021 – 2026), iliyolenga kuimarisha ustawi na maendeleo ya Wazee Nchini; pamoja na kile alichobainisha kuwa katika utekelezaji wake wa vitendo, Serikali imeandaa Sera ya Hifadhi ya Jamii ya Mwaka 2014 ambayo pia imeweka mikakati madhubuti ya kusimamia Maendeleo ya Wazee, hapa Nchini.
Akitoa ufafanuzi juu ya Posho la Wazee, Dokta Mwinyi amefahamisha kwa kusema, "Kwa kuthamini mchango mkubwa wa Wazee wetu katika kuleta maendeleo ya Nchi, Serikali imeongeza Kiwango cha Pencheni Jamii kutoka Shilingi Elfu Ishirini (20,000/=) hadi Elfu Khamsini (50,000/=) sawa na asilimi Mia na Khamsini (150%) kwa Wazee wote wenye umri wa miaka Sabiini (70) na kuendelea ikiwa ni miongoni mwa utekelezaji wa Sera ya Hifadhi yaJamii ya Mwaka 2014 ambayo imeeleza changamoto kubwa inayowakabili Wazee ni ukosefu wa usalama wa kipato; Na kwamba mpaka kufikia Septemba 2023, jumla ya Wazee 29,307 wamesajiliwa, ambapo kwa Unguja ni 17,482 sawa na asilimia 59.6; na 11,825 kwa Pemba, sawa na asilimia 40.3 ambao wanapokea Pencheni kila Mwezi; na kati ya hao Wanawake ni 16,889 sawa na asilimia 57.6, na kwa Wanaumeni 12,418 sawa na asilimia 42.4".
"Napenda kuchukua nafasi hii kuwaagiza watendaji wote wanaoshughulikia suala hili la Pencheni-Jamii kuzidisha ushirikiano, ili kuhakikisha lengo la Serikali linafikiwa, pamoja na kuondosha changamoto zote zinazojitokeza wakati wa usajili hadi kupokea Pencheni- Jamii; Aidha, katika kuhakikisha Mpango huu wa Pencheni-Jamii unaimarika zaidi, Serikali imeandaa Sheria ya Kusimamia Masuala ya Wazee, Namba 2 ya Mwaka 2020 ambayo imeweka Miongozo imara inayohakikisha Wazee wetu wanapatiwa pencheni kwa kuzingatia Vigezo vilivyowekwa".
Rais Dokta Mwinyi, katika Hotuba yake hiyo, amefahamisha kwamba, Serikali inaendeleza jitihada zake za kuwahudumia na kuwatunza Wazee wasiokuwa na Ndugu wala Jamaa, katika Makao Maalum ya Wazee, yaliyopo Sebleni na Welezo kwa Unguja, na Limbani kwa Pemba, ambapo kwa sasa Jumla ya Wazee 63 wanatunzwa katika Makao hayo, huku wakiendelea kupatiwa huduma muhimu zikiwemo Chakula, Malazi, Mavazi, Matibabu na Posho.
Ametoa wito kwa familia na wanajamii kutokwepa majukumu ya kuwalea Wazee na kuwacha tabia ya kuwapeleka kulelewa katika Vituo vya Wazee, kwani wanahitaji huruma na mapenzi kutoka kwa watoto na jamii inayowazunguka, kama ambavyo Vitabu Vitukufu vimehimiza.
Aidha, Dokta Mwinyi ametumia fursa hiyo kuwakumbusha Wazee juu ya Wajibu wao wa kuendelea kutoa maelekezo mema na mawaidha juu ya ustawi mzuri kwa jamii, hasa wakati huu ambao panashuhudiwa mporomoko mkubwa wa maadili.
Akiwa Mgeni Rasmi wa Hafla hiyo, Mheshimiwa Othman ameambatana na Mke wake, Mama Zainab Kombo Shaib.
Naye, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Mhe Riziki Pembe Juma amesema Serikaki imefanikisha kuwepo kwa harakati mbali mbali zikiwemo za kuwafikia Wazee wa Hali tofauti katika jamii, sambamba na kuandaa Makongamano ya kujenga uelewa, ili kuhakikisha Maadhimisho ya Mwaka huu yanafana zaidi na kugusa ngazi zote.
Amehimiza pia haja ya kuwathamini na kuwatunza Wazee, bila ya bughudha wala kuwapa usumbufu, huku akifafanua kwamba tayari Serikali ya Zanzibar imetoa Vitambulisho kwa Wazee waliotiimiza umri wa Miaka 70, ambavyo vitasaidia upatikanaji wa huduma muhimu zikiwemo za usafiri wa umma, afya, Viwanja vya Michezo vya Serikali na Pencheni-Jamii, ambapo hadi sasa takriban Wazee 28,668 wamepatiwa.
Wazee hao, ambao miongoni mwao wamekabidhiwa Vitambulisho kwaniaba ya wenzao kwaajili ya kupata huduma mbalimbali, wamemtunukia Mheshimiwa Rais zawadi, kikiwemo Cheti cha Shukran.
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Mwaka huu ni UTHABITI WA WAZEE KWENYE DUNIA YENYE MABADILIKO, ujumbe unaokwenda sambamba na Lengo Nambari 10 la Maendeleo Endelevu, linalohusu kupunguza tofauti miongoni mwa Nchi na linalolenga kuhakikisha unakuwepo usawa katika upatikanaji wa fursa na kupunguza tofauti ya kipato kupitia mikakati mbalimbali ikiwemo ya maendeleo na ustawi wa Wazee.
Viongozi mbalimbali wamehudhuria Hafla hiyo wakiwemo Mawaziri; Manaibu Waziri; Makatibu na Manaibu Katibu Wakuu wakiongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Mheshimiwa Zena Ahmed Said; Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya; Mabalozi na Wanadiplomasia,; Wakuu wa Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa; Watendaji wa Serikali; Viongozi wa Vyama vya Siasa; Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Wabunge; Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama; Washirika wa Maendeleo; Mabaraza ya Wazee; Wasomi na Wanataaluma; na Asasi za Kiraia.
Hafla hiyo imeambatana na Dua, Utenzi kutoka kwa Bi Amina Mkombe; Ngoma ya Mwanandege ya Kikundi cha Sanaa cha Jeshi la Polisi Zanzibar, pamoja na Tumbuizo za Bendi za Vikosi vya Ulinzi Nchini, baada ya Kukagua Maonyesho ya Bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na Wazee, kupitia Jumuiya zao.
Siku hii inayoadhimishwa ifikapo Tarehe 1 Oktoba ya Kila Mwaka, ilianza kuadhimishwa rasmi mnamo Mwaka 1991, baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la Mwaka 1990 kuketi na Kupitisha Azimio Nambari 45/106 ambalo liliitenga Siku hii Maalum, ili kutambua na kuthamini Mchango wa Wazee Duniani.
0 Comments