Ummulkuthum Omar Daktari Bingwa wa magojwa ya kike na Uzazi kutoka
Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar |
Na Nihifadhi Abdulla Issa:
Dhana ya malezi katika jamii imezoeleka ni pale
mtoto anapozaliwa ndipo hutayarishiwa mfumo wa malezi kwa baadhi ya familia kwa
kupata huduma stahiki ikiwa ni pamoja na malezi na uangalizi wa wazee na jamii
iliomzunguka.
Dhana hii inakwenda mbali zaidi kwa baadhi ya
wanaume na jamii kuona kwamba ujauzito hauhitaji uangalizi na matunzo bali kile
kinachozaliwa ndicho kinachostahiki maandalizi na matunzo .
Tukirudi nyuma kidogo kuangalia Msemo wa Wahenga husema “Kulea mimba si kazi bali kulea mwana ndio
kazi”.
Kwa dunia ya sasa msemo huu hauwendi na wakati
uliopo kutokana na ugumu wa kazi nzito ya kulea mimba kwa mazingira ya wakati
huu na kukabiliwa na vikwazo kadhaa ikiwemo maradhi na magonjwa tofauti ukilinganisha
na zama walizoishi mababu na mabibi zetu.
Hatusemi kwamba kwa wakati huo hakukuwa na maradhi
na magonjwa ingawa ni kwa kiasi kidogo mno ukilinganisha na wakati wa sasa wa
sayansi na teknologia.
MTAALAM WA
AFYA
Wakati jamii ikiamini hivyo kwa upande wa malezi na
huduma kwa mtoto wataalam wa Afya kwa upande wao wana mitazamo yao ya kitaalam
inayoelezea dhana hiyo kwa upana.
Daktari Bingwa wa magojwa ya kike na Uzazi Dk
Ummulkuthum Omar kutoka Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja amesema kwa upande wa Afya ya
Uzazi kiujumla huanzia tokea pale mimba itapotunga kwenye fuko la uzazi hadi
kuzaliwa na hapo ndipo yanapoanza malezi hasa.
Dk Ummulkulthum amesema suala la Afya ya Uzazi
linaanzia mbali sio kama watu wanavyofikiria toka siku mtoto akizaliwa mpaka anakufa
anaishi katika dhana ya Afya ya Uzazi.
“Suala la Afya ya Uzazi si la mwanamke tu bali ni la
mtoto wa kike na wa kiume kwa sababu huwezi kuzaa bila ya mwanamme, hivyo hata
katika malezi na makuzi ya mtoto ni lazima kushirikiana kwa pamoja kwa mustakabali
wa ustawi wa mtoto kiakili na hata kimwili, Dkt Ummulkuthum Omar Daktari Bingwa
magonjwa ya kike na Uzazi.
MUAMKO WA WAZAZI
Fatma Juma 27 mkaazi wa Kinuni Mkoa wa Mjini
Magharib amesema mume wake hajapata Elimu ya Afya ya Uzazi hali inayopelekea
kutokuwajibika ipasavyo katika majukumu ya pamoja ya kulea mimba na hata watoto.
“Mume wangu hana taalum ya Afya ya Uzazi yeye
anachojuwa ni kutafuta kula ndio jukumu lake na akifanikiwa ndio hilo limeisha
ila masuala ya kushiriki katika mambo ya nyumbani kama vile kunisaidia kazi za
nyumbani anasema sio jukumu lake kwa sababu akitoka asubuhi kwenda kazini mpaka
usiku.
Mohd Ali 43 mkaazi wa Maungani anasema mtoto ni
lazima alilewe kwa mashirikiano ya wazazi wa pande zote ila inakuwa ni kikwazo
kwa sababu majukumu kwa wananume yanakuwa ni mengi anatakiwa kutoka kwenda
kutafuta mahitaji ya nyumbani.
“Mimi ni mzazi na nawajibika kulea sikatai lakini ni
lazima kutoka asubuhi kwenda kazini kutafuta mahitaji na mke wangu ndio anabaki
na watoto kwa ajili ya malezi na majukumu ya nyumbani,” alisema.
Baadhi ya wazazi wanawake walikuwa na mawazo tofauti
kwamba kutokana na hali ya sasa imebadilika tofauti na zamani , kwa sababu
wazee wote wawili wanatika kwenda kazini kutafuta maisha kutokana na ugumu wa
maisha.
“Mimi ni mama wa watoto watatu lakini pia ni
mfanyakazi, nalazimika kutoka asubuhi kuwahi kazini kutekeleza majukumu mengine
na kuwaacha watoto wangu na mlezi, alisema mzazi.
Rukayya Aali Hassan mkaazi wa Kwahani 36 anasema kutokana na hali ya maisha ya sasa imebadilika
hivyo imesababisha watoto kukosa muda stahiki wa malezi kwa wazazi ama jamaa
zao wa karibu kama ilivyokuwa hapo awali (zamani).
“Mzee wangu alikuwa anafanya kazi ni muajiriwa
Serikalilini, ni Mwalimu wa Skuli sisi tumezaliwa tisa lakini tulilelewa na bibi
yetu mzaa mama, wakati mama anakwenda kazini bibi yupo nyumbani analea wajukuun
zake,” alisema Rukayya.
Bakar Faki 25, mkaazi wa Fuoni Unguja amesema
wanaume wana jukumu la kutoka nje kwenda kutafuta matumizi ya mke na watoto
kama vile chakula na mahitaji mengine ya lazima hivyo jukumu la malezi na mambo
ya nyumbani ni wajibu wa mwanamke ambae umemuowa.
“ Nikitoka asubuhi mpaka asubuhi kwa hiyo changamoto
za malezi kwa mchana wa kutwa zinamkuta mwanamke, nikirudi napewa kesi
nasuluhisha ndo maisha tuanayoishi mimi na mke wangu,” alisema Bakar.
DINI YA KIISLAM INASEMAJE KUHUSU JUKUMU LA MALEZI
SHEIKH KHAMIS ABDULHAMID
Malezi ya mtoto huanzia mbali tokea taratibum za
kutafuta mchumba hadi kufikia ndoa yenyewe na utekelezaji wa majukumu yake
ipasavyo.
Sheikh Khamis Abdulhamid kutoka Baraza la Maulamaa
Zanzibar akizungumzia mada juu ya malezi
ya watoto katika Uislam alianzia mbali na kusema katika kitabu kitukufu cha QUR
AN kimeeleza wazi kuhusu jambo hilo,
Sheikh Khamis alitaja Sura mbali mbali za QUR AN kama
vile Suratul Nnisai na Hujrat zinazungumzia malezi ya watoto kwa kusema
Mwanamme ni mlezi au msimamizi kwa mwanamke na si Kiongozi na majukumu ya
nyumba ni ya mwanamme na asiesimamia ana dhambi na atalipwa.
“Baadhi ya wanaume wanatafsiri vibaya aya hii hata
kama mwanamke anafanya kazi ni hisani yake tu kukupa bali si wajibu wake,”
Sheikh Abduhamid .
Aidha Aalim huyo alisema Baba ndio mwenye jukumu la
kulea watoto na akenda kinyume na wajibu aliopewa basi sheria za Allah za
zitamkamata.
Akifafanua kuhusu ndoa amesema suala la Ndoa ni
Sheria pia ni Sunna lakini hubadilika kuwa dhambi endapo hutoitendea haki akithibitisha
maneno hayo kutoka katika kitabu kitakatifu QUR AN Suratul Annur, Aya ya 33.
“Wajizuie wale wanaume kutokuowa mpaka atakapowapa
uwezo Mola wa,” Sheikh Khamis Abdulhamid.
Hata hivyo amesema Suratul Talaqa imetoa ufafanuzi
mzuri kuhusu haki ya mwanamke na mtoto (yaani malezi ) wakati wa kumuacha mke
kumpatia haki zake ikiwa ana mtoto
anaenyonyesha mtoto wako ni wajibu kumlipa (kumpa fidia).
“ Ikiwa ndani ya ndoa si lazima kumlipa bali
mukiachana ikiwa atakunyonyeshea mwanao sheria ya dini ya Kiislam inasema
umlipe,” Sheikh Khamis.
Sheikh Khamis Abdulhamid kutoka Baraza la Maulamaa Zanzibar |
SKULI ZINAZOTUMIKA KWA UANGALIZI KWA MTOTO (BABY
CARE)
Mkuu wa Taaluma wa Skuli ya Pasira ilioko Kianga, Mkoa
wa Mjini Magharibi, Wilaya ya Magharibi ‘’A” Deleta Said Othman amesema skuli
hizo wazazi wanapeleka watoto wao kutokana na kukosa muda muafaka wa kulea
wakiwa wafanyakazi (wameajiriwa).
Othman amesema muamko wazazi kuwapeleka watoto
katika skuli hizo hutegemea malezi na mtoto kufundishwa kujitegemea mwenyewe
ukilinganisha na kumpeleka kwa mlezi wa kawaida hupata malezi tu bali na
kufundishwa kujitegemea na kufanya baadhi ya mambo yake mwenyewe kama vile baada ya kula kuondosha sahani yake
mwenyewe.
“Kulea watoto wadogo ni kazi lakini tunakumbana na changamoto mbali mbali
kama vile kwenye mfumo mzima wa chakula mfano unampa uji analia lakini pia
kuzoea mazingira watoto hulia sana, na wanahitaji uangalizi wa hali ya juu kwa kwa sababu hupokea maradhi mara moja
ukilinganisha na watoto wakubwa hiyo inabidi uache kazi kuwashughulikia,”
Deleta Othman, Mkuu wa Taaluma Pasira.
Hata hivyo Othman amesma katika vituo hivyo wataalam
wa Afya hupita mara mbili mpaka tatu kwa mwaka kuangalia Afya ikiwemo usafi wa
vyoo na mazingira halisi ili kuwalinda watoto na athari zinazoweza kujitokeza
kiafya.
MFANYAKAZI KATIKA SKULI YA PASIRA
Zulfa Khamis 30 ni mama wa watoto watatu mkaazi wa
Mwera anasema kazi ya ulezi ni ngumu hasa ukizingatia watoto bado ni wadogo
sana hawajaweza kujitambuwa na wengine hata kuzungumza hawajajuwa vizuri kwa
hiyo inatuwia vigumu uache kazi ufanye kazi.
“Watoto ni wadogo sana kuanzia miaka miwili wana
kazi sana, kazi ya ulezi si lele mama ujipange na ndio maana baadhi ya wazazi
huwapeleka watoto wao kwenye vituo vya kulelea kwa sababu ulezi ni kazi nzito,”
alisema Zulfa.
MTAALAM WA SAIKOLOJIA
Kutokana na tatizo la kulelewa watoto nje ya familia
zao au vituo vya kulelea watoto huathiri akili ya mtoto mwenyewe na familia kwa
ujumla na hata ukuwaji wake kwa sababu wanahitaji uangalizi wa hali ya juu.
Mtaalam wa Saikolojia Amina Khalfan kutoka Hospitali
ya wagonjwa wa Akili Kidongo Chekundu Wilaya ya Mjini anasema watoto kuwa mbali
na familia zao au watu waliowazoea huleta athari kwao kwa ukuwaji lakini hata
kiakili.
“Watoto wanakabiliwa na upweke kwanza, lakini hata
kubadilishwa mazingira mpaka kuyazoea inachukuwa mda na vile vile huga tabia za
watu wengine wapya waliowazunguka na si za familia zao kama zamani tulivyolele
sisi,” Alisema Amina, Mtaalam wa Saikolojia.
Chanzo cha watoto kutolelewa na wazazi au watu wao
wa karibu kunachangiwa na sababu kadhaa zikiwemo za kiuchumi na hata mogogoro
ya familia kama vile kuachana kwa baba na mama na mtoto kulelewa na mzazi mmoja
hivyo ipo haja kwa jamii kukaa chini na kuangali akwa namna gani kulitafutia
ufumbuzi ama muarubaini tatizo hili kwa kuokowa nguvu kazi ya Taifa.
Mradi wa Afya ya Uzazi Wasichana na Wanawake
umefadhiliwa na Shirika la Wellspring Philanthropic Fund la Marekani.
Kwa sasa mradi huu unatekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari
Wanawake kwa Upande wa Bara na Zanzibar kwa lengo la kuongeza ushawishi na
utetezi kwa kupitia vyombo vya habari juu ya umuhimu wa upatikanaji wa huduma
ya Afya ya Uzazi kwa wasichana na wanawake
0 Comments