Ticker

6/recent/ticker-posts

Watu Wenye Ulemavu Zanzibar Wawezeshwa Kiuchumi

 

Na Nafda Hindi Zanzibar

Chama cha Waandishi wahabari wanawake Tanzania TAMWA,ZNZ kwa kushirikiana na Shirikisho la Jumuiya ya watu wenye ulemavu Zanzibar (SHIJIWAZA) kimetowa muongozo wa kupanga,kuchaguwa na kusimamia biashara kwa watu wenye mahitaji maalum hususan watu wenye ulemavu.

Akiwasilisha muongozo huo mkufunzi na mtaalam wa mambo ya vikundi Abuubakar Othman amesema muongozo huo utasaidia watu wenye ulemavu kufanya shughuli zao mbali mbali za ujasiria mali kwa lengo la kujikwamua na utegemezi.

Amesema muongozo huo umejikita zaidi kuangalia mambo muhimu kwa watu wenye ulemavu ikiwemo kujuwa tabia na desturi za watu wenye ulemavu mjini na vijijijni na kutengeneza mazingira ya kujiona wako pamoja nao. Aidha muongozo huo pia umejikita kuonesha muda, zana na vifaa vya kufundishia ikiwemo kadi maalum zenye michoro ya picha na hata kuonesha alama ili waweze kufahamu kwa haraka na kufanya kwa vitendo kile watakachosomeshwa.

“Muongozo huo pia ndani yake muna michezo ya kuigiza,hadithi, kazi za nyumbani na za darasani ili kuwarahisishia walengwa kuweza kufahamu wale wanaosomeshwa,” alisema Abuubakar.Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Jumuiya ya Watu wenye ulemavu Zanzibar (SHIJIWAZA) Mwan-dawa Khamis amesema muongozo huo utasaidia watu wenye ulemavu kujua namna ya kujishughulisha na masuala ya miradi .

Hata hivyo amesema katika muongozo huo kumejitokeza changamoto kama vile kuonesha mbinu tofauti za ufundishaji ikzingatiwa kuna watu wenye ulemavu tofauti tofauti ni vyema kila kundi kuiainishiwa vifaa husika kulingana na aina ya ulemavu alionao.

“Ni fursa kubwa kwa watu wenye ulemavu na wanapaswa kuichangamkia na itawasaidia kiuchumi kutokana na kundi hilo wanaishi katika mazingira magumu endapo watachangamkia fursa hiyo wataondokana na umaskini,” alisema Bi Mwan-dawa.

 

Nae Mkurugenzi wa Mtendaji wa Jumuiya ya watu wenye ulemavu Zanzibar (UWZ ) Shaib Abdalla Mohammed amesema muongozo huo ni mzuri ila unahitaji kuangaliwa kwa kina na kuhakikisha mapungufu yaliyomo kufanyiwa marekebisho kwa lengo la kuwasaidia wanufaika wa mradi wa kunufaika kiuchumi hususan watu wenye ulemavu Zanzibar.

“Haya mambo ni mchakato na ndio maisha hivyo ni fursa kwa watu wenye ulemavu pamoja na familia hivyo historia ya vikundi Zanizbar inaonesha kutokuwa na uadilifu, hivyo kuwepo utaratibu maalum ya kuwabana wahusika,” alisema Shaib.

Mradi wa KIJALUBA ISAVE ni mradi Jumuishi Unaofanywa na TAMWA,ZNZ kwa kushirikana Shirikisho la Jumuiya ya watu wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJIWAZA) unaolenga kuwawezesha watu wenye ulemavu kiuchumi ambao ni wa majaribio katika Wilaya mbili, Kusini kwa Unguja na Chake Chake kwa Pemba.


Post a Comment

0 Comments