Na Ahmed Abdulla
Kamati ya ushauri ya utekelezaji wa mradi wa VIUNGO
Zanzibar (ZMAG) imesema jamii visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla inaweza
kuepuka maradhi mbalimbali iwapo wataacha kutumia vyakula vinavyotumia mbolea
ya kemikali wakati wa uzalishwaji wake na kutumia vyakula vinavozalishwa kwa
kupitia mbolea za asili wakati wa uzalishaji wake (Organic food.)
Ushauri huo umetolewa na wajumbe wa kamati ya
ushauri na wadau mbalimbali wa masuala ya kilimo wakati wa kikao cha kuangalia
ni namna gani mradi VIUNGO unaendelea kutekelezwa na kuleta mabadiliko katika
sekta ya kilimo cha mbogamboga,matunda na viungo ili kuleta tija kwa pande
zote.
Mkutano huo uliofanyika katika ofisi za wizara ya
kilimo Maruhubi Zanzibar na kuwashirikisha wadau kutoka taasisi tofauti
zikiwemo za Seikali, mashirika yasio ya kiserikali na wakulima .
Wakichangia mada zilizowasilishwa katika mkudano huo
ndugu Ali Abdalla kutoka CFP alisema
kuna idadi kubwa ya wananchi kwenye jamii bado hawajaelewa umuhimu wa kutumia
vyakula vinavozalishwa na mbolea asili na ndio maana hadi leo wananchi
walio wengi huendelea kutumia vyakula vinazozalishwa kwa kutumia kemikali jambo
ambalo ni hatari sana kwa afya na ardhi.
Alisema tafiti mbali mbalimbali zinazonesha watu
wengi hupata maradhi tofauti na imebainika kuwa chanzo cha maradhi hayo ni
kutumia vyakula ambavyo uzalishwaji wake hutumia mbolea nyingi zisizokua za
asili na ndio chanzo cha matatizo mengi hivi sasa.
Alieleza kuwa licha ya kuwa suala la uelewa ni
tatizo linalosababisha wananchi kutumia bidhaa hizo lakini pia alisema baadhi
yao hufuata urahisi wa bidhaa zinazozalishwa kupitia mbolea ya kemikali
ukilinganisha na mbolea za asili ingawa alisema hazofautiani sana ukichunguza
kwa undani.
Katika hatua nyengine mtalamu kutoka wizara ya
kilimo Zanzibar Omar Abuubakari alisema wakulima wengi Zanzibar na
Tanzania wamekua wakiendenlea kutumia mbolea za kemikali kwa kile
wanachokiamini kwamba uzalishaji mkubwa zaidi wa mazao yao kinyume na matumizi
ya mbolea za asili.
Alisema kwa mazingira hayo jitihada zaidi
zinahitajika ikiwemo utoaji wa elimu kwa jamii ili iweze kutambua umuhimu
wa kutumia chakula kilichozalishwa kwa kutumia mbolea za asili.
Kwa upande wake Dkt.Mzuri Issa alisema wakati
wanaendelea kufikiri kuhusu hali hiyo kuna umuhimu mkubwa kutazama pande
zote mbili ukizingatia mbolea za kemikali ni biashara ambayo inategemewa na
wengi.
Alisema suala muhimu zaidi ni jamii kupewa elimu ili
waweze kufahamu madhara ya utumiaji wa vyakula vinavyozalishwa kwa kutumia
mbolea za kemikali na kuoneshwa faida za kutumia mbolea za asili.
Akifafanua zaidi alisema anaamini kupitia mfumo
huo utaweza kutoa elimu kwa kina na kuwaacha wananchi kuamua wenyewe ni
mazao gani wanahitaji kutumia katika maisha yao ya kila siku.
Akieleza kuhusu baadhi malengo ya mradi wa VIUNGO
meneja mkuu wa mradi huo wa VIUNGO Amina Ussi khamis alisema ni kuwawezesha
wakulima Unguja na Pemba kupitia njia bora za kilimo.
Pia alisema ni kuwainua baadhi ya akina mama
ambao ni wanufaika wa mradi huo ikiwemo kuwapa elimu ya kuwanzishwa kwa vikundi
vya kuweka na kukopa ili waweze kukidhi shughuli zao za kila siku.
Aidha alisema malengo mengine ni kufungua fursa
kupitia mnyororo wa thamani kutoka kwa wakulima hadi kwa mlaji, ambapo
anaamini kuwa una fursa nyingi ambazo zinaweza kuingiza kipato kwa kila mtu
ambae ni mnufaika wa mradi huo.
Mradi wa VIUNGO ni wa miaka minne ambao umelenga
kuwafikia wanufaika zaidi ya 57,000 kwa Unguja na Pemba na unaotekelezwa na
taasisi tatu ikiwemo People Development Forume,Community Forest in Pemba (CFP)
pamoja na Tanzania Media Women Association TAMWA-ZNZ kwa ufadhili Jumuia
ya Ulaya (EU)
0 Comments