Ticker

6/recent/ticker-posts

Sababu Za Kutokufikia Lengo Kwa Wajasiriamali Zaanikwa

 


Mwezashaji kutoka wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Pemba akitoa mafunzo ya jinsi ya kutumia mbinu bora za kulinda na kukuza biashara kwa wajasiriamali


Imeelezwa kwamba wajasiriamali kukosa taaluma ya mbinu za ufuatiliaji na usimamizi wa biashara zao ndiyo chanzo kwa biashara hizo kushindwa kukua na hata kupelekea kufa kabisa kwa biashara.

 

Hayo yamebainishwa na mkufunzi wa masuala ya ujasiriamali kutoka wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na uchukuzi Pemba, Faki Othman Faki wakati wa mafunzo ya siku moja kwa wajasiriamali 25 kisiwani Pemba juu ya mbinu za ukuzaji wa biashara na shughuli za wajasiriamali.

 

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tznazania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kupitia mradi wa kuwawezesha wanawake kiuchumi alisema licha ya kuwepo kwa idadi kubwa ya wanaojiingiza katika shughuli za ujasiriamali lakini wengi wao wanashindwa kusonga mbele kutokana na kukosa misingi ya elimu ya usimamizi wa shughuli hizo.

 

“Tunashudia wengi wakianzisha shughuli nyingi za ujasiriamali kwa kasi lakini baada ya siku chache wanasitisha na kurudi nyuma kutokana na udhaifu wa kukosa utaalamu wa usimamizi wa shughuli zao.,” alisema.

 

Aliongeza kwamba, “tatizo kubwa lililopo kwa wajasiriamali wengi wanakosa jicho la kuona madhaifu yao katika uendeshaji wa shughuli na kupelekea kukata tamaa ya kuendelea na shughuli husika pale wanapokumbana na vikwazo na kukimbilia kuanzisha shughuli nyingine pasipo kufanya tathimini yoyote.”

 

Aidha aliwataka wajasirimali kuhakikisha wanazingatia misingi minne ya ujasiriamali ili kujitofautisha sokoni kwa lengo la kuwavutia zaidi wateja wao kuendelea kutumia huduma wanazozalisha.

 

Alisema, “Ili mjasiriliamali aweze kupiga hatua katika shughuli za ujasiriamali lazima azingatie mambo makuu manne ambayo ni fursa, changamoto, nguvu na udhaifu.”

 

Pia Faki aliwasisitiza wajasiriamali hao kuachana na utaratibu wa kujifungia na kuwaamulia wateja bidhaa za kuwauzia na badala yake  wafanye tafiti ndogo kabla ya kuzalisha bidhaa ili kutambua mahitaji ya wateja wao kwa wakati husika.

 

“Tatizo lingine walilonalo wajasiriamali wengi ni kuamua wenyewe kitu cha kuuza. Nikuombeni tusiwachagulie wateja kitu cha kununua badala yake tunatakiwa tuwasikilize wateja wetu nini wanahitaji, uwezo wao kiuchumi, sehemu ya kuuzia, na njia ya kuwauzia bidhaa zetu, kwa kufanya hivyo hakuna bishara ya mjasiriamali itakayofeli.”

Afisa uwezeshaji wanawake kiuchumi kutoka TAMWA Nairat Abdalla Ali

 

Mapema afisa uwezeshaji Wanawake kiuchumi wa TAMWA ZNZ,  Nairat Abdalla Ali, alisema mafunzo hayo ni mwendelezo wa TAMWA ZNZ kupitia mradi huo unaofadhiliwa na Milele Zanzibar Foundation kuwawezesha wajasiriamali kuwa na elimu ya masoko ili kuhimili matakwa ya wateja sokoni.

 

“Huu ni mwendelezo wa kukumbushana kuhusu mbinu bora za uzalishaji na uuzaji wa bidhaa tunazozalisha kwa kuzingatia matakwa ya wateja ili tuweze kufikia malengo ya kujiinua kiuchumi na kuondokana na changamoto zinazotukabili katika jamii,” alisema

 

Rashid Khamis Othman mjasiriamali mshiriki wa mafunzo alisema mpango wa kutolewa kwa mafunzo hayo yameanza kuwaimarisha kibiashara na kupata uwezo wa kukabiliana na changamoto za uzalishaji pamoja na kutambua fursa za masoko katika jamii kulingana na hali zao.

 

“Baada ya kupata elimu ya ujasiriamali tulifanya utafiti na kugundua kwamba wateja wengi hawana uwezo wa kununua ndoo nzima ya tungule (nyanya) hivyo tukabadili mfumo wa uuzaji kwa kuzigawa kulingana na uwezo wa mnunuzi,” alisema.

 

Aliongeza, “TAMWA ZNZ ni wakombozi wetu katika masuala ya ujasirimali, mwanzo tulikuwa tunauza tungule kwa bei ya hasara lakini baada ya kuanza kutumia mfumo wa kuuza kulingana na uwezo wa mteja husika kulingana na elimu ya masoko tuliyonayo tumepandisha mauzo kutoka laki mbili kwa shamba lakini saizi kila tukilima kwa shamba la ukumbwa ule ule hatupungui milioni moja,” alisema.

 

Mafunzo hayo ya siku moja yamejumuisha wajasiriamali kutoka Wilaya za mikoa ya Kusini na Kaskazini Pemba ambazo mradi wa kuwawezesha wanawake kiuchumi (WEZA III) unatekelezwa.


Post a Comment

0 Comments